

Kuna lugha ambayo imekuwa ikitumika sana katika jamii na watoa huduma za afya wamekuwa wakikiuka au wakijisahau juu ya swala hilo; matumizi ya lugha kama ''meza vidonge viwili mara tatu'', mtu mwingine anaweza kutafsiri kama umeze vidonge viwili muda wowote ili mradi tu ufikishe mara tatu, pamekuwa na ukosefu wa elimu juu ya baada ya muda gani unapaswa kumeza au kutumia dawa zako unapokuta lugha kama hiyo, hata ikitokea umesahau maelekezo uliyopewa lakini yameandikwa.
Ifahamike kuwa, kutokumeza dawa kwa muda unaotakiwa inaweza kuwa moja ya sababu ya kushindwa kupona na huchangia usugu wa vimelea ambukizi juu ya dawa (drug resistance) hata kama kweli ulimeza mara tatu au mara mbili kama ilivyotakiwa, hivyo ni muhimu kuelewa alama hizi. Swali ni je umeze dawa hiyo kila baada ya muda gani?.
Ifuatayo ni mifano ya namba zionekanazo katika cheti cha dawa au maelekezo ya dawa kutoka kwa mtoa huduma za afya hasa mfamasia na maana zake;
Dawa ambayo ni kidonge
1 x 1 : Meza kidonge kimoja kila baada ya saa ishirini na nne (24)
2 x 1 : Meza vidonge viwili kila baada ya saa ishirini na nne (24)
3 x 1 : Meza vidonge vitatu kila baada ya saa ishirini na nne (24)
1x 2 : Meza kidonge kimoja kila baada ya saa kumi na mbili (12)
1 x 3 : Meza kidonge kimoja kila baada ya saa nane (8)
1 x 4 : Meza kidonge kimoja kila baada ya saa sita (6)
↑ ⤷--- Chukua saa 24 gawa kwa namba hii, utapata kila baada ya muda gani utumie dawa
Idadi ya vidonge
Kama umesoma kwa makini, utagundua kuwa namba ya mwanzo kabisa (iliyopo mkono wako wa kushoto) inamaanisha idadi ya vidonge, namba inayofuatia inamaanisha mara ngapi dawa hiyo imezwe kwa siku moja.
Kwa hesabu rahisi kabisa, siku moja ina masaa ishirini na nne, hivyo ukichukua namba ambayo ipo mkono wa kulia kwako ukagawa, utapata kila baada ya muda gani unapaswa kumeza dawa hiyo, mfano ukikuta imeandikwa kuwa: 1 x 4 maana yake ni meza kidonge kimoja (1) kila baada ya saa sita ( 24 ÷ 4 = 6).
Ikiwa 2 x 3, maana yake meza vidonge viwili (2) kila baada ya saa nane ( 24 ÷ 3 = 8).
Dawa za maji
Maelezo ni sawa na dawa za kidonge, tofauti ipo katika kiasi cha dawa lakini maelezo ya baada ya muda gani unywe dawa hiyo ni sawa. Mfano;
5ml x 2: Maana yake, meza mililita tano za dawa kila baada ya masaa kumi na mbili ( 24 ÷ 2 = 12),
10ml x 3: Meza mililita kumi (10ml) kila baada ya saa nane (24 ÷ 3 =8).
Ikumbukwe kuwa, kumeza dawa kila baada ya saa husika (time interval) ni muhimu ili kupata matokeo yanayotarajiwa kila utumiapo dawa. Kila inapotokea umesahau, soma maelekezo uliyoandikiwa na mfamasia wako au ukishindwa kabisa wasiliana na mfamasia wako au mtalaam wa afya.
No comments:
Post a Comment