
Kila dawa ina masharti yake, yasipozingatiwa kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kupata matokeo yanayotarajiwa. Watu wamekuwa wakipuuzia sana juu ya muda wa kumeza dawa, pamoja na hilo nimekuwa nikiulizwa maswali mengi sana juu ya nini cha kufanya unaposahau kumeza dawa. Wengine wanauliza; je nikisahau kumeza dawa na muda wa dozi nyingine umekaribia, nimeze dozi mbili au nisubili au moja, au dozi nzima imeharibika kwa hiyo niachane nayo na nianze upya?

Inapotokea umesahau kumeza dawa, unatakiwa unywe dawa pale tu unapokumbuka, hautakiwi kumeza dozi mbili kwa wakati mmoja ukidhani kuwa unafidishia dozi uliyosahau kumeza, kufanya hivyo kutakusababisha ongezeko la madhara yatokanayo na dawa hali inayoweza kupelekea kudhoofu kwa afya yako (dawa ni sumu ikitumika kinyume na maelekezo). Pale tu unapokumbuka kuwa umesahau kumeza dawa, meza dawa mara moja, na kisha endelea na dozi zingine zinazofuata kwa mujibu wa maelekezo ya mtaalamu wa afya, hivyo utamaliza dawa zako kwa muda unaotakiwa.
Ikitokea umekumbuka kuwa ulisahau kumeza dawa na pia muda wa dozi inayofuata umekaribia mfano, dakika 30, au saa 3, basi subiri na meza dozi inayofuata na endelea kutumia dawa yako kwa mujibu wa maelekezo ya mfamasia au mtaalamu wa afya, kwa hiyo mfano, dawa uliyokuwa unameza kila baada ya saa 12 kwa siku tano (5), kama ulianza kumeza asubuhi, ulitakiwa kumaliza dawa zako jioni, kwa sababu ulisahau kumeza dozi moja, hivyo utamaliza kutumia dawa siku ya sita asubuhi (kwa sababu ya dozi moja).
Ikumbukwe kuwa, kila dawa ina sifa zake za kipekee na madhara yake na matokeo yake hutofautiana. Hivyo basi, usisite kuwasiliana na kupata ushauri wa kitaalamu kila uwapo na wasiwasi juu ya nini ufanye.