Message from Authors

We give valuable information to optimize and promote rational use of medicine in popular language. Information is a powerful tool that can benefit or harm the public, we bring you information to benefit and promote health. If you do not understand Swahili, highlight the content and translate to any language to get the intended message. Follow us, subscribe and ask any question for help. Karibu.

Monday, 17 July 2017

JE NI DAWA ZOTE ZINAMUINGILIANO HASI NA MAZIWA?

Maziwa ni moja ya chanzo muhimu sana ya lishe katika mwili wa binadamu na wanyama pia. Maziwa yana madini mengi, mafuta, vitamini pamoja na protini ambazo kwa ujumla wake zinafaida nyingi sana, na hivyo wagonjwa na wasiowagonjwa wanapaswa kunywa maziwa kila siku. Watu wanaogopa kunywa maziwa yawe ya mtindi au ''fresh'' pindi wanapougua na kutumia dawa. Maziwa ni muhimu sana kwa mtu mgonjwa.
Watu wengi wamekuwa wakiaminishwa kwamba, ukimeza dawa na kunywa maziwa ndani ya muda mfupi, basi, dawa hiyo/hizo haziwezi kufanya kazi. Je kuna ukweli ndani ya mapokeo hayo?.

Kabla ya kutoa jibu, nitaelezea muingiliano wa dawa na maziwa ni kitu gani. Muingiliano wa maziwa na dawa ni pale ufanisi/ utendaji kazi wa dawa unapungua au kuongezea baada ya kumezwa muda mfupi baada au kabla ya kunywa maziwa. Kupungua au kuongezeka kwa utendaji kazi wa dawa baada ya kunywa maziwa unategemea sana katika aina ya dawa. Na hivyo tunakuwa na aina mbili za matokeo, matokeo hasi kama ufanisi utapungua, na chanya kama ufanisi utaongezeka au utaboreshwa.

Je maziwa yanaathiri vipi utendaji kazi wa dawa?
Chanzo kikuu cha muingiliano wa dawa na maziwa ni madini yaliyomo katika maziwa yajulikanayo kwa jina la kitaalamu kama ''Calcium''. Katika mwili, madini haya yanafanya kazi ya kuimalisha mifupa na meno, ufanyaji kazi ya misuli na mfumo wa fahamu. Unapokunywa maziwa muda mfupi baada ya kumeza dawa, madini haya kuchangamana na dawa na kutengeneza kitu ambacho hakiwezi kupenya katika kuta za tumbo na kuingia kwenye damu kwa ajili ya utendaji kazi yake. Hali hii hupelekea kuwa na kiasi kidogo sana cha dawa katika damu hali ambayo inaweza kuleta matokeo hasi mfano, kutokupona (kwa sababu wadudu hawajafa), kuongeza uwezekano wa wadudu kuwa sugu dhidi ya dawa.

Je ni dawa zipi zina muingiliano hasi na maziwa? 
Kuna dawa nyingi zenye muingiliano hasi na maziwa, na hivyo ni vyema kumuuliza mfamasia anaekupa dawa hizo, ili kujua kama kuna muingiliano au la. Baadhi ya dawa zenye muingiliano na maziwa ni;
  • Dawa zenye jamii ya ''ciprofloxacin'' dawa hii inajulikana sana kutibu homa ya tumbo na ile hali ijulikanayo sana katika jamii kama mkojo mchafu.
  • Dawa zenye jamii ya ''Tetracycline'' dawa hii ilijulikana sana kipindi cha nyuma kama rangi mbili.  
Unashauriwa; kunywa maziwa masaa matatu (3) hadi manne (4) baada au kabla ya kumeza dawa. Pia ikumbukwe kuwa si maziwa tu yanaweza kuleta muingiliano huu, bali hata bidhaa au chakula kilichoandaliwa na maziwa kama ''yoghurt'' inaweza kuleta matokeo yale yale.
 
Je ni dawa zipi zina muingiliano chanya na maziwa, na kitu gani kinasababisha mwingiliano huo? 
Ieleweke kuwa, kila dawa ina sifa zake za kipekee na hivyo baadhi ya dawa zikimezwa na maziwa au muda mfupi na maziwa, basi ufanisi wa dawa hizo huongezeka, na hivyo ni vyema kuongea na mfamasia wako ili kujua. 
Maziwa ni moja ya chanzo kikubwa cha mafuta (fats), baadhi ya dawa huihitaji sana mazingira ya uwepo wa mafuta futa katika kuta za tumbo ili ziweze kupenya kwa urahisi na kuingia damuni, uwepo wa dawa ya kutosha katika damu inapngeza ufanisi wa dawa. Mfano wa dawa kama hizo ni dawa maarufu sana kwa jina la mseto (Artemether lumefantrine) au ALU inayotumika kutibu ugonjwa wa malaria. Unashauriwa kumeza dawa hizo na maziwa au kunywa maziwa muda mfupi baada ya kumeza dawa zenye jamii hiyo, dawa hizo hazidhuriwi na madini yaliyo katika maziwa.

Hivyo basi, si kila dawa inaathiriwa ikimezwa muda mfupi kabla au baada ya kunywa maziwa, ni vyema kuijua dawa unayomeza, ili uweze kufahamu kama inamuingiliano hasi au chanya ikimezwa pamoja na maziwa. Muulize mfamasia wako ili kupata taarifa sahihi. 


No comments:

Post a Comment